Reputation Management
CPR certification onlineCPR certification online

 

Mwaka mmoja kabla ya kumaliza shahada yangu ya juu kabisa (PhD) nilipata bahati ya kutembelea moja wapo ya kituo kikubwa kabisa cha mazoezi ya olympic mjini Roma, Italia. Kituo au chuo hiki kinajulikana kwa jina la SCUOLA DELLO SPORT. Nilikuwa pale kwa takribani wiki mbili, kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo, ikiwa ni pamoja na kufuatilia maisha ya wanamichezo wanaojiandaa kushiriki katika mashindano ya Olympic.

Kiukweli nilijifunza mambo chungu nzima ikiwa ni pamoja na nidhamu ya hali ya juu waliyokuwa wakionyesha wanamichezo hao katika kipindi chote nilichokuwa pale.

Ninaposema nidhamu simaanishi kufuata kile anachosema mwalimu au coach; la hasha, hapa namaanisha nidhamu katika muda, mpangilio wa mazoezi, mapumziko na juu ya yote mpangilio wa LISHE au ulaji kwa ujumla.

Kikubwa nilichokipata pale ni ukweli kwamba ushindi si bahati na wala si miujiza bali ni matokeo ya maandalizi ya hali ya juu yanayohusisha nidhamu isiyo ya kawaida katika kufanya mazoezi, kupumzika na kula.

 

Kwa muda mrefu sasa nimekuwa nikifuatilia (japo si moja kwa moja) maandalizi ya baadhi ya timu na hata wanamichezo mbali mbali na kugundua mambo chungu nzima ambayo kiukweli kama hayatarekebishwa na kufanyiwa kazi, swala la ushindi au kupata wachezaji wengi bora kama Mbwana Samata, litabakia kuwa ndoto. Ikumbukwe kwamba haya ni maoni yangu binafsi, ninayoyatoa kutokana na utashi wa taaluma yangu, na hayahusishwi na timu au mwanamichezo yeyote. 

LICHA YA JUHUDI KATIKA MAZOEZI, LISHE KWA WANAMICHEZO HUUPUUZWA

Ili kujenga timu na wanamichezo wenye uwezo ni muhimu kuzingatia lishe maalumu kwa wanamichezo

Nilichokiona ni ukweli kwamba, japo timu na wanamichezo wengi hujitahidi sana katika mazoezi (nasisitiza hujitahidi ila wanaweza kuboresha zaidi) swala la lishe halijapewa kipaumbele hata kidogo. Ikumbukwe kwamba kibailojia mazoezi huchangia asilimia thelathini (30%) tu katika ukakamavu na ufanisi wa mwanamichezo husika (fitness and performance), wakati lishe huchangia kiasi kilichobaki (asilimia sabini (70%)). 

Maana yake ni kwamba, kama timu yako au wewe binafsi unazingatia mazoezi peke yake, na kutokujali lishe kabisa–hauhusishi asilimia sabini (70%) ya jambo ambalo linaweza kukuletea mabadiliko chanya. Kwa maana nyingine mabadiliko chanya kwako ni ndoto, au yakitokea ni bahati tu.  

Nguvu inayohitajika kwa ajili ya mazoezi na michezo hutokana na lishe. Misuli inayotumika kwa kiasi kikubwa wakati wa michezo hujengwa pia na lishe bora. Moja kwa moja utaona lishe ni muhimu sana, licha ya uhusiano kati ya lishe na mazoezi kuwa kama ule wa kuku na yai.

Ikumbukwe kwamba kioo chetu ni timu kubwa kama vile Real Madrid, Manchester United na zinginezo. Na kwa haraka haraka utakubaliana na mimi kwamba timu hizi zimeajiri wataalamu wa lishe ili wapangilie lishe za wachezaji wao. Wakati timu zetu hutumia nguvu zote kutafuta walimu (coaches), sidhani kama kuna timu inayodhani kuwa na mtaalamu wa lishe kuna umuhimu wowote kwa timu. Kwa maana hiyo, huhitaji shahada kutambua kwamba itakuwa vigumu kwa wachezaji wa timu hizi kufikia viwango vya wachezaji wa timu kubwa kama Manchester United.

Christiano Ronaldo ni mchezaji mwenye wapenzi wengi duniani kote, halikadhalika hapa nchini kwetu. Hebu tupate mhutasari wa lishe ya Christiano Ronaldo kama ilivyoandikwa na James Gold.

 

James Gold anasema, Christiano Ronaldo ni mchezaji mahiri na mwenye mafanikio makubwa katika soka. Pamoja na jitihada kubwa katika mazoezi, na kuimarisha uwezo wa miguu yake, Christiano huzingatia sana nguvu, ufanisi, stamina na kasi. Kufanikisha haya yote Ronaldo huzingatia lishe bora na kama ilivyo kwa wachezaji wengine wote, Ronaldo anaye mtaalamu mahiri wa lishe ambaye hupangilia milo yake. Ufuatao ni mhutasari wa mpangilio wa mlo wa Christiano Ronaldo.

 1. Hula mara nyingi kwa siku: Mlo wa siku wa nyota huyu umegawanywa katika milo sita (6) iliyotenganishwa kwa kati ya masaa mawili (2) mpaka manne(4). Hii ni muhimu ili kuongeza ufanyaji kazi wa mwili (body metabolism). Ronaldo anasema, ussiruhusu masaa manne yapite bila kutia chochote tumboni.

 2. Hula mlo wenye kiasi cha kutosha cha protini: Mlo wa Ronaldo unahusisha kiasi kikubwa cha minofu (lean meat) ambayo ni muhimu kwa kujenga misuli

 3. Hutumia virutubisho lishe (Nutritional supplements) kwa ajili ya kuupumzisha mwili na kuurudisha katika hali yake baada ya michezo (recovery): Ronaldo hutumia vinywaji vya protein (protein shakes), virutubisho kwa ajili ya kupooza viungo na mchanganyiko wa vitamini.

 4. Hutumia mboga mboga kwa wingi: Kwa kuwa mboga mboga zina vitamini na madini mengi ambayo ni muhimu kwa kupooza na kupumzisha mwili (recovery)

 5. Hukwepa vyakula vyenye sukari: Vyakula na vinywaji vyenye sukari nyingi husababisha mwili kutunza mafuta kitu ambacho kuzorotesha ufanyaji kazi wa mwili.

 Huu hapa mfano wa mpangilio wa mlo wa Christiano Ronaldo

 

KIFUNGUA KINYWA

Mchanganyiko wa nafaka zisizokobolewa (mtama au ngano), weupe wa yai (egg white) na juice fresh ya matunda (bila sukari).

 

CHAKULA CHA MCHANA

Makaroni ya ngano isiyokobolewa, mboga mboga, viazi vya kuokwa na kachumbari iliyochanganywa na minofu ya kuku (chicken salad).

 

ASUSA (SNACKS)

Kipande cha jodari katika mkate (Tuna roll) na juice ya matunda hususani juice ya malimao.

 

MLO WA USIKU

Wali na mikunde, kidari cha kuku au bata mzinga, maharage na matunda.

 

VIRUTUBISHO LISHE (NUTRITIONAL SUPPLEMENTS)

Kinywaji cha protini (Whey protein shake) na mchnganyiko wa vitamin

Ni muhimu kupata elimu na ufahamu kuhusu virutubisho lishe (supplements) vilivyomuhimu kwa wanamichezo

 

Endapo wewe ni mwanamichezo au kiongozi wa timu na unazingatia hayo, hongera na endelea kujitahidi na mazoezi. Endapo husingatii lishe bora, itakuwa vigumu sana kuwa mkakamavu. Jifunze kuhusu lishe ya michezo (sports nutrition).

 

 

Ref:

  1. http://www.borntoworkout.com/cristiano-ronaldo-training-workout-routine-diet-plan/
  2. http://www.thehealthsite.com/news/cristiano-ronaldo-fitness-and-diet-regime/

 

 

Free Presentantion on ...

Free Presentation on Weight Loss with Zohra ...

+ View

Recent Articles

Utastaajabishwa na ...

Wakati mwingine tunakata tamaa kufanya mambo ...

+ View

Matatizo sugu yanayo ...

Wengi wetu tunafahamu umuhimu wa mazoezi katika ...

+ View

MEN’S BELLY FAT: Pride ...

The fact that abdominal fat, or belly fat, is not ...

+ View
  • Prev
  • Sponsor this Section
Scroll to top