Reputation Management
CPR certification onlineCPR certification online

Mbwa na paka ni wanyama wanaopendwa na kufugwa majumbani kwa sababu mbalimbali. Bila shaka umewahi, au huwa unapishana na mbwa au paka katika mitaa unayoishi au unayotembelea. Wakati mwingine wanyama hawa wanaweza kuwa wamebeba virusi hatari vinavyosababisha ugonjwa wa Rabies ambao umepewa jina la kichaa cha mbwa.

Ugonjwa huu huathiri wanyama wengi wakiwemo mbwa, na kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya duniani (WHO) zaidi ya asilimia 90% ya wagonjwa huambukizwa rabies kwa kung’atwa na mbwa.Ugonjwa wa kichaa cha mbwa ni ugonjwa hatari unaoathiri mfumo wa fahamu na kusababisha kifo. Ugonjwa huu husababishwa na maambukizi ya virusi yanayotokea pale unapong’atwa na mbwa au paka mwenye virusi hivi. Kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania ugonjwa huu hutokana na kung’atwa na mbwa wasiopatiwa chanjo. Kwa nchi zilizoendelea maambukizi mengi hutokana na kung’atwa na wanyama wa mwitumi kama popo, mbwa mwitu n.k.

Virusi vinavyosababisha ugonjwa huu hukaa kwenye mate ya mnyama mwenye maambukizi. Hivyo mtu aliyepata maambukizi anaweza pia kumuambukiza mwingine iwapo atamng’ata au mate yake yataingia sehemu yenye jeraha. Ugonjwa huu ni hatari na hauna tiba, na hivyo husababisha kifo kwa kila mgonjwa anayepata maambukizi. 

Kwa mujibu wa maelezo ya mkuu wa idara ya magonjwa ya watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili Dr Mary Charles, tangu mwezi January mpaka mwisho wa mwezi Agosti (miezi 8) watoto 7 walilazwa wakiwa na ugonjwa huu, baada ya kung’atwa na mbwa. Walipatiwa matibabu ila wote walipoteza maisha.”

Tafiti zilizofanywa Tanzania zinaonyesha ni asilimia 17% ya mbwa ndiyo wamepatiwa chanjo. Hii inaonyesha uwezekano mkubwa wa kuwepo kwa mbwa wenye maabukizi ya virusi hivi hatari. Mbwa anatakiwa apatiwe chanjo kila mwaka, na anakuwa anafunguliwa kadi maalum kwa ajili ya kuhifadhi kumbukumbu za chanjo. Unapong’atwa na mbwa, unashauriwa kama unamfahamu mmiliki wake, mwombe akupatie kadi ya chanjo ya mnyama wake kwa ajili ya kuionyesha hospitali. Kama mbwa ni wa mtaani asiye na mmiliki, basi inashauriwa kumtafuta ili afanyiwe uchunguzi kama ana dalili za maambukizi. Ugonjwa wa kichaa cha mmbwa huathiri mfumo wa fahamu.

Nini dalili za ugonjwa huu?

Mtu aliyeng’atwa na mbwa au paka mwenye maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa huu huonyesha dalili kati ya siku 20-90 kutegemeana na sehemu ya mwili iliyong’atwa. Kama jeraha lipo kichwani au shingoni dalili za ugonjwa hutokea mapema zaidi ikilinganishwa na pale jereha linapokuwa mguuni. Kawaida virusi vya huu ugonjwa husafiri kwenda kwenye ubongo kupitia mishipa ya fahamu iliyo katika sehemu ya mwili jeraha lilipotokea.

Dalili za awali: hutokea siku 2-10 baada ya kupata maambukizi. Hizi ni pamoja na kujisikia uchovu, kichefu chefu, kichwa kuuma, homa, kusikia baridi, kutapika,kuharisha na kukosa usingizi.

Dalili za kuathirika kwa mfumo wa fahamu na ubongo: katika hatua hii ya ugonjwa, mgonjwa huwa na kutetemeka kwa misuli na anaweza kupata degedege. Mgonjwa anaweza kuwa mkali, asiyetulia (restless), asiyejitambua (confusion) na anaweweseka na kuongea vitu visivyoeleweka (hallucinations). Pia mgonjwa huwa na tabia ya kung’ata watu walio karibu. Huwa wana fujo za muda mfupi zinazoweza kuchukua dakika tano kisha hutulia.

Wagonjwa hawa hawataki kabisa maji wala upepo kama wa feni (hasa unaolekeka usoni mwao). Wanapoona maji hujisikia vibaya, wakati mwingine hujisikia vibaya hata wakisikia neno maji likizungumzwa.

Baadaye wagonjwa hawa hupoteza fahamu na hufariki kutokana na athari za ugonjwa kwenye ubongo.

Matibabu ya ugonjwa

Matibabu ya mtu aliyeng’atwa na mbwa anayesadikiwa kuwa na ugonjwa wa kichaa cha mbwa ni pamoja na

 • Kusafisha jeraha
 • Kutoa chanjo ya rabies (rabies vaccine and Immunoglobulin)
 • Kupatiwa matibabu kulingana na dalili zitakazojitokeza 

Kujikinga na ugonjwa wa kichaa cha mbwa: hatua zifuatazo zitasaidia kujikinga na ugonjwa huu

 • Wafundishe watoto kuepuka kucheza na mbwa au paka wa mitaani (stray dogs and cats)
 • Kuhakisha mbwa na paka wako wamepatiwa chanjo ya kuwakinga na ugonjwa wa kichaa cha mbwa (rabies)
 • Kutoa taarifa kwa afisa mifugo unapoona mbwa au paka mwenye dalili za ugonjwa au anayoonekana kuwa na tabia zisizo za kawaida
 • Kuhimiza jirani zako nao kuhakikisha wamewapatia chanjo mbwa na paka wao kila mwaka au kadiri ya maelekezo ya afisa mifugo
 • Kwa wale wanaofanya kazi ya kukutana na mbwa au paka wanatakiwa wapatiwe chanjo ya kuwakinga na ugonjwa huu

Kwa kuwa ugonjwa huu ni hatari ni jukumu letu sote kuhakikisha tunahimizana na kushawishi kupitia kwa wawakilishi wetu wa serikali za mitaa kuhakikisha mbwa wetu wamepata chanjo ya kuzuia ugonjwa wa rabies.

Dalili saba za mbwa mwenye uwezekano wa kuwa na ugonjwa wa kichaa cha mbwa (rabies)

 • Mbwa kuwa mpweke na kukaa sehemu moja kwa muda mrefu bila kufanya chochote. Wakati mwingine huangalia sehemu moja kwa muda mrefu bila kuangalia sehemu nyingine
 • Anakimbia kimbia hovyo kwa muda mrefu
 • Anakuwa mkali zaidi na anaweza kumvamia anayemtunza kama mtu asiyemfahamu
 • Anakuwa mkorofi wala hafuati maelekezo
 • Anang’ata kitu chochote kilicho mbele yake ikiwemo chuma, matairi, mifugo hata watu (maambukizi ya ugonjwa)
 • Ukimwita anageuka huku masikio yake yamenyanyuka juu, masikio na manyoya kumsimama kama anajiandaa kukuvamia
 • Ulimi huning’ing’inia nje na hutoa mate na udenda mwingi

Ukiona dalili hizi kwa mbwa wako au kwa mbwa yoyote barabarani toa taarifa kwa afisa mifugo wa wilaya (veterinary officer) au kituo cha polisi kilicho jirani. Mbwa wenye dalili hizi wanatakiwa kuuawa kwa kuwa hakuna dawa ya kutibu ugonjwa wa rabies.

 

Free Presentantion on ...

Free Presentation on Weight Loss with Zohra ...

+ View

Recent Articles

Utastaajabishwa na ...

Wakati mwingine tunakata tamaa kufanya mambo ...

+ View

Matatizo sugu yanayo ...

Wengi wetu tunafahamu umuhimu wa mazoezi katika ...

+ View

MEN’S BELLY FAT: Pride ...

The fact that abdominal fat, or belly fat, is not ...

+ View
 • Prev
 • Sponsor this Section
Scroll to top