Reputation Management
CPR certification onlineCPR certification online

 UGONJWA WA SHINIKIZO LA DAMU NINI: Huu ni ugonjwa unaotokana na kuongezeka kwa ukinzani katika mpito wa damu katika mishipa ya damu inayosambaza damu kutoka katika moyo kwenda sehemu nyingine za mwili. Iwapo shinikizo la damu (blood pressure) yako limefika milimita za zebaki 140/90 kwa vipimo viwili katika siku tofauti basi una tatitzo la shinikizo la damu

NINI CHANZO CHA SHINIKIZO LA DAMU:

 • Chanzo cha shinikizo la damu hakifahamiki kwa zaidi ya 90% ya wagonjwa. Tafiti zimeonyesha uwepo wa vinasaba vya kurithi vinavyosababisha ugonjwa huu. Hili linaonekana wazi kwa jinsi ugonjwa huu unavyoathiri watu wa familia moja, mfano watoto wa baba au mama mwenye huu ugonjwa wana uwezekano mkubwa wa kupata ugonjwa kuliko wale wasio na historia ya huu ugonjwa kwenye familia zao.

 • Asilimia 10% ya wagonjwa wa shinikizo la damu kama madhara ya magonjwa mengine, kwa mfano ugonjwa wa figo husababisha shinikizo la damu kuwa kubwa.

   

NINI DALILI ZA UGONJWA: Kwa kawaida shinikizo la damu halina dalili maalum, hivyo wagonjwa hawana dalili zozote. Wagonjwa wachache wanaweza kuwa na maumivu ya kichwa, kuwa na uono hafifu na kujisikia uchovu. Dalili nyingi hutokana na madhara yanayosababishwa na ugonjwa huu, mfano moyo kwenda mbio, kuchoka haraka (ugonjwa wa moyo); kuvimba miguu (ugonjwa wa moyo na figo), kupata ulemavu wa upande mmoja (ugonjwa wa kiharusi). Na pale dalili hizi zinapotokea zinaashiria ugonjwa umekuwepo kwa muda mrefu na kusababisha madhara hayo.

VITU GANI VINAWEZESHA KUPATA HUU UGONJWA:

Kuna mambo yanayochochea uwezekano wa kupata tatizo la shinikizo la damu, hasa kwa watu wenye historia ya huu ugonjwa kwenye familia zao, mambo haya ni kama ifuatavyo:

 

 • uzito mkubwa wa mwili (unene)

 • tabia ya kutofanya mazoezi

 • kutumia vyakula vyenye mafuta mengi; mfano vitu vya kukaangwa kwa mafuta mengi

 • kutumia kiasi kikubwa cha chumvi

NINI CHA KUFANYA KUEPUKA MADHARA YA HUU UGONJWA: ukifanya mambo yafuatayo utaweza kujiepusha na ugonjwa huu au madhara yanayotokana na huu ugonjwa

 • Jenga tabia ya kupima afya yako walau mara moja kwa mwaka, hakikisha unajua kiwango cha shinikizo la damu (BP) yako.

  • Iwapo BP yako ni 140/90 mmHg au zaidi, nenda kapime tena na kama itaonekana kuwa juu mara ya pili inaashiria una tatizo la shinikizo la damu (hypertension).

 • Zingatia kanuni za afya ya mwili wako ikiwa ni pamoja na

  • Kupunguza uzito wa mwili wako kama ni mkubwa

  • Jenga tabia ya kufanya mazoezi

   • Tumia ngazi badala ya lift, hasa unaposhuka kutoka ghorofani kwenda chini

   • Egesha gari lako mbali kidogo na ofisi yako ili upate fursa ya kutembea kwa miguu kwenda ofisini kwako.

  • Punguza matumizi ya vyakula vyenye mafuta mengi

   • Epuka matumizi ya vyakula vilivyokaangwa kwa mafuta mengi

   • Tumia zaidi vyakula vilivyochemshwa bila kuwekwa mafuta kwa wingi

  • Punguza ulaji mkubwa wa vyakula vya wanga; mfano viazi, ugali, wali

   • Vyakula vya wanga hugeuzwa kuwa mafuta na kuhifadhiwa mwilini, hivyo tumia vyakula hivi asubuhi na mchana ili viweze kutumika na kupunguza uwezekano wa kuhifadhiwa mwilini.

   • Wakati wa jioni kabla ya kwenda kulala ni vizuri ukatumia zaidi mboga za majani, matunda na vyakula vya protini (mfano kuku na samaki)

  • Punguza matumizi makubwa ya chumvi, hasa chumvi inayoongezwa wakati wa kula chakula mezani

NINI CHA KUFANYA IWAPO UNA UGONJWA WA SHINIKIZO LA DAMU: iwapo kwa bahati mbaya umepatikana na tatizo la shinikizo la damu zingatia yafuatayo

 • Badili mfumo wa maisha yako ili kuweza kuudhibiti ugonjwa huu na kuepuka madhara yeke kwa;

  • Kupunguza uzito wa mwili kama una uzito mkubwa

  • Kupunguza matumizi ya vyakula vilivyokaangwa kwa mafuta mengi

  • Kupunguza matumizi ya chumvi nyingi

  • Kufanya mazoezi mara kwa mara, inashauriwa kufanya mazoezi kwa dakika thelathini kila siku

 • Zingatia matumizi ya dawa za kushusha shinikizo la damu kama utakavyoshauriwa na wataalamu wa afya, kumbuka

  • Dawa zinashusha tu shinikizo la damu, ili kukukinga na madhara ya shinikizo la damu

  • Ukiacha kutumia dawa shinikizo la damu litapanda na kuwa juu tena. Kila unapoacha kumeza dawa unajiweka katika hatari ya kupata madhara ya ugonjwa huu yakiwemo kiharusi (stroke), ugonjwa wa figo (renal failure), ugonjwa wa moyo (heart failure)

 • Pima shinikizo la damu (BP) mara kwa mara ili uone kama limekaa sawa

  • Ukiwa unatumia dawa shinikizo la damu linatatkiwa liwe chini ya 140/90

  • Kwa wagonjwa wa kisukari wanatakiwa kuhahakikisha shinikizo la damu linakuwa chini wakati wote kwa kuwa wana hatari zaidi ya kupata madhara ya ugonjwa wa shinikizo la damu.

 • Hakikisha unamuona daktari wako kila baada ya miezi mitatu, na unafanya vipimo kuona kama kuna madhara yoyote yametokea kutokana na shinikizo la damu

  • Kipimo cha mkojo kuangalia kama kuna protini ambayo ni kiashiria cha awali cha kuathirika kwa figo, pima kila baada ya miezi 6 au kadiri ya ushauri wa daktari wako

  • Kipimo cha damu cha kuangalia ufanyaji kazi wa figo, serum creatinine, pima kadiri daktari wako atakavyokushauri ili ni vizuri kipimo kifanyike walau mara moja kwa mwaka

  • Fanya kipimo cha moyo (echo) walau mara moja kwa mwaka au kadiri daktari wako atakavyokushauri.

  • Muone daktari wa macho kuangalia kama kuna madhara ya shinikizo la damu kwenye macho.

 

NI MUHIMU KUZINGATIA MAMBO YOTE YALIYOTAJWA HAPO JUU KWA SABABU ZIFUATAZO:

 • Ugonjwa huu hauna dalili, na watu wengi hutambua wana tatizo hili baada ya kupata madhara makubwa hususani haya yafuatayo

  • Kupata ugonjwa wa moyo (heart failure)

  • Kupata ugonjwa wa figo (renal failure), figo zote mbili zinashindwa kufanya kazi hivyo utahitaji upate huduma za kusafisha damu kwa mashine (dialysis) kwa maisha yako yote au upate mtu wa kukupa figo (renal transplantation)

  • Kiharusi (stroke) ambao utakupa ulemavu wa maisha

 • Ukibadili mfumo wa maisha yako, ukitumia dawa kama utakavoshauriwa utaweza kuishi maisha yako vizuri na kuepuka madhara ya ugonjwa huu.

Free Presentantion on ...

Free Presentation on Weight Loss with Zohra ...

+ View

Recent Articles

Utastaajabishwa na ...

Wakati mwingine tunakata tamaa kufanya mambo ...

+ View

Matatizo sugu yanayo ...

Wengi wetu tunafahamu umuhimu wa mazoezi katika ...

+ View

MEN’S BELLY FAT: Pride ...

The fact that abdominal fat, or belly fat, is not ...

+ View
 • Prev
 • Sponsor this Section
Scroll to top