Reputation Management
CPR certification onlineCPR certification online

 

Picha hii ya mzee Juma Kulwa Kuliwa miaka michache kabla hajapata tatizo hilo la kiafya

Mzee Juma Kulwa Kuliwa (1950) ni mkazi wa Tabora, alipata ugonjwa uliopelekea kufanyiwa operesheni kubwa kuondoa sehemu ya taya la juu iliyokuwa imeharibika kwa ugonjwa unaoitwa “Osteomyelitis”. Ugonjwa huu huharibu mfupa na matibabu yake yanategemea na usugu wa tatizo, huweza kuhusisha matumizi ya dawa ya kuua bakteria (antibiotics) pekee, au pamoja na upasuaji wa kuondoa sehemu ya mfupa iliyoharibika. Mzee Kulwa alifanyiwa upasuaji na kuondolewa sehemu ya taya la juu. Baada ya matibabu haya alipata changamoto ya kula na kuongea na thamani ya maisha ilikuwa duni sana (reduced quality of life). Hata hivyo baada ya wataalamu kumtibu sasa, imemrudishia thamani yake ya mwanzo. Hili hapa simulizi lake

 

Picha: Mzee Kulwa kabla ya kufanyiwa upasuaji kuondoa sehemu ya taya la juu.

Jamii Health: Pole sana mzee Kulwa kwa tatizo lako hilo

Mzee Kulwa: Asante sana

Jamii Health: Wewe ni mwenyeji wa wapi?

Mzee Kulwa: Mimi mwenyeji wa Tabora mjini, mtaa wa Mwanza Road.

Jamii Health: Jamii Health Magazine tunajishughulisha na kutoa elimu ya afya kwa umma, na mojawapo ya dhamira yetu, ni kuongea na watu waliopitia matatizo makubwa kama ya kwako, ili kuweza kutoa ujumbe utakaowasaidia na wengine. Unaweza kueleza tatizo lako lilianzaje?

Mzee Kulwa: Tatizo lilianza mwaka 2008, niligundulika kuwa na kisukari nikaanza kutumia dawa. Mwaka 2010 mwezi wa nane, sukari ikawa juu sana na hii ikanipelekea kulazwa hospitali mara nne ndani ya miezi miwili katika hospitali ya Kitete, Tabora. Pia kichwa kilikuwa kinauma sana hasa upande mmoja wa kushoto, na eneo lote la uso upande huo ulipata ganzi. Kutokana na hali hii ndugu na jamaa waliokuwa wakiniuguza waligawanyika mtazamo, kuna ambao walikuwa wanashauri niende kupata tiba ya kienyeji, na wengine wakataka niendelee kutibiwa hospitalini. Kutokana na kutopata nafuu baadhi ya ndugu walifikiria kunihamishia hospitali nyingine. Hapa kukatokea mvutano, kuna baadhi ya ndugu walishauri nisihangaishwe niachwe nifie nyumbani badala ya kupelekwa mbali. Mwishowe mke wangu na baadhi ya ndugu walinihamishia hospitali ya misheni Ndala kinyume na matakwa ya ndugu wengine. Nikiwa hospitali ya Ndala kwa siku kadhaa uvimbe ukatokea upande wa kushoto usoni. Nilipewa dawa bila mafanikio hapo hospitalini nilipokuwa nimelazwa. Uvimbe ulikuwa kama jipu na uliongezeka kwa haraka sana, na maumivu yalikuwa makali sana. Jipu hilo liliiva na kupasukia mdomoni, na usaha ukawa unatokea mdomoni na puani upande wa kushoto. Madaktari wakashauri nipewe rufaa kuja Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Jamii Health: Ulipata changamoto gani baada ya kupata rufaa?

Mzee Kulwa: Changamoto kubwa ilikuwa upande wa familia. Kulianza mvutano kati ya pande mbili; mmoja ukataka nipelekwe kwa waganga wa kienyeji kwa ajili ya matibabu, na upande mwingine ukataka nije kutibiwa hapa Muhimbili. Hatimae upande uliotaka nije kutibiwa Muhimbili ulishinda. Changamoto nyingine mwaka huo (2010) ulikuwa wa uchaguzi, na kipindi nilichopata rufaa kilikuwa kipindi cha uchaguzi. Usafiri wa kuja Dar ulikuwa mgumu sana. Changamoto nyingine ni namna ya kusafiri, maana mimi nilikuwa mtu wa kulala, nilikuwa siwezi kukaa kwa muda mrefu, lakini hakukuwa na namna nyingine, nilichoka sana. Niliondoka tarehe 4/11/2010 kwa basi la abiria lililokuwa likitokea Mwanza, nilibahatika kupata kiti cha mwisho kabisa mimi na mke wangu na tulifika Dar es salaam mida ya saa tatu usiku. Asubuhi ya tarehe 5/11/2010 ndio tulikuja Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Jamii health: Pole sana, ni kawaida ukiugua tatizo linakuwa la kijamii sio la mtu binafsi. Baada ya kuja Muhimbili nini kiliendelea?

Mzee Kulwa: Siku ya tarehe 5/11/2010 nakumbuka ilikuwa siku ya ijumaa nililazwa na nilipata huduma, upasuaji mdogo ulifanyika na kutoa usaha. Kisha daktari akaandika vipimo vingine zaidi pamoja na kuchukua kipimo kwa ajili ya kansa. Meno ya upande huo wa kushoto yalikuwa yamelegea sana, upande ambao kipimo kilichukuliwa kupelekwa maabara. Hata hivyo majibu ya vipimo vyote yalikuwa mazuri, hakukuonekana tatizo lililosababisha huo uvimbe na usaha na meno kulegea. Baadae kwenye raundi ya wodini wakashauri nifanye kipimo cha CT scan. Majibu yakaonyesha kuwa mfupa wa shavu na taya la juu upande wa kushoto vimeharibika, wakaniambia natakiwa nifanyiwe upasuaji. Nilifanyiwa upasuaji, nakumbuka nilipelekwa chumba cha upasuaji saa sita mchana, na nilipozinduka nilijikuta nipo chumba cha wagonjwa mahututi na nimewekea mrija wa chakula na bandeji usoni.

 

Picha: mzee Kulwa baada ya upasuaji wa kuondoa sehemu ya taya la juu, upande wa kushoto, akiwa analishwa kwa njia ya mrija

Jamii Health: Nini kilifuatia baada ya upasuaji?

Mzee Kulwa: Nilikuwa siwezi kuongea, nilikuwa natumia kalamu kuandika ili kuwasiliana. Chakula nilikuwa napewa kwa njia ya mrija. Maisha yalibadilika kabisa. Hata baada ya kutoa mrija nilikuwa siwezi kutamka maneno, na kula nilikuwa nakula vyakula vilaini kwa shida sana. Niliruhusiwa kutoka hospitali na kwenda nyumbani nikapewa tarehe ya kurudi. Pia nilielekezwa kuja kumwona daktari wa afya ya kinywa na meno. Nilipofika hapa nikapokelewa vizuri na nikachukuliwa vipimo vya awali na kupewa tarehe ya kurudi. Zoezi hili nalo lilichukua muda, wakati mwingine nilikuwa naenda nyumbani Tabora na kurudi huku Dar, kila ninapopangiwa kuja. Baada ya miezi sita ndio nikapata kifaa hiki kinachonisaidia kuongea vizuri na kula bila shida, na maisha kuwa yamerudi kawaida sasa, na muonekano wangu uko mzuri ukilinganisha na baada ya upasuaji.

Picha: inavyoonekana mdomoni baada ya upasuaji wa kuondoa sehemu ya taya la juu. Picha inaonyesha uwazi unaoweka mawasiliano kati ya pua na mdomo baada ya paa la kinywa kuondolewa kwa sehemu. Hii ndio ilimsababishia changamoto ya kutamka maneno, na kumeza chakula.

Jamii Health: Ulivyorudi nyumbani Tabora ilikuwaje?

Mzee Kulwa: Kwanza watu hawakutegemea kuniona tena. Na kuna baadhi ya marafiki ambao walikuwa karibu na mimi kabla sijaugua, ila baada ya kupata matatizo haya wamejitenga nami kabisa mpaka sasa. Niliporudi nyumbani kwa mara ya kwanza, wakati bado sijapata kifaa hiki kinachonisaidia, nilikuwa siwezi kuongea, ila familia ilifarijika sana kuwa walifanya uamuzi sahihi kunipeleka hospitali ya rufaa. Pengine leo nisingekuwa hapa kuongea na wewe kama ningepelekwa kwa mganga wa kienyeji, maana tatizo lenyewe bila operesheni lisingeisha.

 

Picha: inaonyesha kinywani baada ya kuwekewa kifaa cha kumsaidia kuongea, kula na kurudisha muonekano wake. Kifaa hiki kinaziba uwazi uliokuwepo na kufunga mawasiliano yaliyokuwepo kati ya pua na mdomo.

Jamii health: Una maoni gani kwa watanzania kwa ujumla?

Mzee Kulwa: Kwanza kabisa jamii ijenge tabia ya kupima afya zao mara kwa mara, ili kugundua tatizo mapema. Mimi mwenyewe nilikuwa na dalili za kuchoka sana na mwili kukosa nguvu, kiu kikali, kukojoa mara kwa mara, macho kukosa nuru, kutoka jasho sana, kusikia njaa sana na homa za mara kwa mara. Siku moja nilipokuwa nimezidiwa sana, nilipelekwa hospitalini ndio nikagundulika nilikuwa na ugonjwa wa kisukari. Maoni yangu ni kuwa watu wazingatie sana matibabu yanayotolewa katika hospitali zetu, na wasipende kukimbilia kwenye tiba za kienyeji.

Jamii Health: Mzee Kulwa asante sana kwa ushirikiano wako

Mzee Kulwa: Asante daktari kwa kunipa nafasi niwaeleze watanzania juu ya historia ya ugonjwa wangu. Napenda kumshukuru Mungu kwa kunipatia uhai na kuniwezesha kupita kipindi hiki cha kuugua kwa uvumilivu. Shukrani za pekee ziwaendee madaktari na wauguzi wa hospitali ya Kitete na Ndala mkoani Tabora na Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu na msaada walionipatia na ambao wanaendelea kunipa hata sasa. Mwisho kabisa kwa namna ya kipekee napenda kumshukuru sana mke wangu, na ndugu na jamaa na marafiki wote walionisaidia katika safari hii ya matibabu kwa michango yao mbali mbali ya hali na mali, bila ya msaada wao nisingeweza mimi mwenyewe.

 

Picha: mzee Kulwa anavyoonekana sasa

Hitimisho.

Mzee Kulwa ameshauri watu wawe na tabia ya kufanya uchunguzi wa afya zao mara kwa mara kama madaktari wanavyoshauri. Pia amesisitiza sana kuwa watu wapatapo matatizo kama haya wasikimbilie kwa waganga wa kienyeji waende hospitali, na wakiwahi wanaweza kupata msaada mapema na kuepuka madhara zaidi yatokanayo na kuchelewa kupata tiba stahiki mapema.

 

Picha hii inaonyesha Kushoto: Mwandishi wa Jamii Health; Dr Deogratias Kilasara,; Kulia Mzee Juma Kulwa Kuliwa

Mzee Kulwa anapatikana kwa namba ifuatayo 0783292593

Free Presentantion on ...

Free Presentation on Weight Loss with Zohra ...

+ View

Recent Articles

Utastaajabishwa na ...

Wakati mwingine tunakata tamaa kufanya mambo ...

+ View

Matatizo sugu yanayo ...

Wengi wetu tunafahamu umuhimu wa mazoezi katika ...

+ View

MEN’S BELLY FAT: Pride ...

The fact that abdominal fat, or belly fat, is not ...

+ View
  • Prev
  • Sponsor this Section
Scroll to top